![]() |
Mwal. Mede |
Baadhi ya mambo yanayoweza kufanyika ili kushinda vita vinavyoweza kuinuka kazini ni:-
1. Kusimama katika Utakatifu na Haki
Kutompa adui nafasi ya kutuonea kwa sababu ya dhambi au udhaifu wa maadili kazini. Kama Danieli, ambavyo walimtafuta kwa bidii lakini hawakumpata na kosa.
Waefeso 6:14 - “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani.”
“Kujifunga kweli viunoni” → Kuishi katika ukweli wa Mungu; kuwa mwaminifu na waaminifu katika kila jambo.
“Dirii ya haki kifuani” → Kuishi maisha ya haki na utakatifu yanayokulinda dhidi ya mashambulizi ya kiroho.
2. Kukiri Neno la Mungu Juu ya Kazi Zetu
Neno la Mungu ni silaha. Litamke kila siku mahali pa kazi. Litatengeneza mazingira ya kibali na ushindi.
Isaya 54:17 - “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa; na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa na hatia. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”
- “Kila silaha haitafanikiwa” → Hakuna mipango mibaya dhidi yako itakayoshinda.
- “Kila ulimi utauhukumu” → Maneno mabaya, fitina au mashtaka hayatadumu; ukweli utashinda.
- “Ni urithi wa watumishi wa Bwana” → Ulinzi huu ni ahadi kwa wale wanaomtegemea Mungu.
3. Kujifunza Kunyamaza na Kumuamini Mungu
Usikimbilie kulipiza au kujitetea kila mara. Wakati mwingine, ushindi hutokea kwa kunyamaza na kumwachia Mungu apigane kwa niaba yako.
Kutoka 14:14 - “Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”
- “Bwana atawapigania” → Mungu mwenyewe anachukua jukumu la kupigana kwa ajili yako katika changamoto zako.
- “Nanyi mtanyamaza kimya” → Unaitwa kuwa na imani, utulivu, na kutokuogopa—kumtumaini Mungu bila hofu.
4. Kutumia Nguvu ya Maombi
Vita vya kazini mara nyingi ni vya kiroho. Kila jambo linaloonekana lina chanzo kisichoonekana. Ombea mazingira ya kazi yako kila siku.
2 Wakorintho 10:4 - “Maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome.”
- “Si za mwili” → Vita vyetu si vya nguvu za kibinadamu (hasira, ugomvi, ujanja)
- “Zina uwezo katika Mungu” → Nguvu yetu inatoka kwa Mungu kupitia maombi, imani, na Neno lake
- “Kuangusha ngome” → Mungu anaweza kuvunja vikwazo vikubwa—hofu, mawazo mabaya, fitina, au changamoto nzito.
I. Omba Kibali na Mafanikio Kutoka kwa Mungu
Kibali hufanya kazi kuwa rahisi. Ukiwa na kibali kutoka kwa Mungu, hata waliokusudia kukuangusha watakusaidia.
Zaburi 5:12
“Kwa kuwa wewe, Bwana, utambariki mwenye haki; kwa kibali chako utamzunguka kama ngao.”
II. Omba Ulinzi Dhidi ya Uchawi na Mipango ya Giza
Wengine wanatumia nguvu za giza kwenye kazi, na mojawapo ya sababu za chuki kuinuka ni pale ambapo watu kutoka madhabahu mbalimbali mnapokutana mahali pamoja. Wenye madhabahu za kipepo, uchawi na ushirikina wanapokutana na watoto wa kweli wa Mungu wanainua chuki na chuki yao kubwa ni kwa sababu zile madhabahu zao zinakuwa zinakosa nguvu mbele ya watoto wa Mungu waliopo makazini.
Ndiyo maana kuna watu kazini watakuchukia, watataka uondoke kwa sababu ya yule aliyepo ndani yako ni mkuu kuliko madhabahu zao, kazi zao za kipepo na kishetani zinakosa nguvu. Ndiyo maana siyo kila vita inayoinuka kazini ni ya mwilini, bali ni ya rohoni na wewe unatakiwa kuwa rohoni kwa kuomba.
Ombea damu ya Yesu kazini na kwenye jina lako la kazini, damu ya Yesu ifunike sura yako, mahali ambapo unakaa.
Ufunuo 12:11
“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo...”
